Inasemekana kundi la wanaharakati wa kimtandao wa ‘the Anonymous’ wamefanikiwa kudukua data kutoka mtandao wa TTCL. Data za wafanyakazi 64,000 zawekwa wazi.
Kundi la kimataifa na la kisiri la wanaharakati wa ‘the Anonymous’ hutumia njia za udukuzi (hacking) kama njia yao ya uharakati na ushinikizi wa jambo wanaloamini.
Kwa sasa kundi hilo linafanya oparesheni wanayoiita #OPAfrica na inahusisha udukuzi wa mitandao ya serikali za Afrika.
Video yao kuhusu oparesheni ya #OpAfrica;
Inasemekana kupitia udukuzi walioufanya kwa tovuti ya TTCL – www.ttcl.com, wamefanikiwa kudukua data za wafanyakazi 64,000 wa shirika hilo. Na data hizo zina vitu kama majina, namba za simu, barua pepe na kwa baadhi hadi nywila (password) zao wanazotumia kuingilia kwenye sehemu ya wafanyakazi katika mtandao huo. Pia kingine kilichokuwepo ni nafasi ya kazi na sehemu (department) ya kazi katika shirika hilo.
Walipoulizwa sababu ya kufanya udukuzi huo kwa mtandao wa TTCL kundi hilo lilisema jambo hilo ni moja kati ya juhudi zao katika vita yao dhidi ya unyanyasaji wa watoto, utoaji ajira kwa watoto, rushwa pamoja na uhuru wa huduma za intaneti.
“Anonymous will always stand against child abuse and child labour, we also won’t let governments play with the citizens anymore, therefore we decided to attack the state-owned telecom company. The corrupt government of Tanzania should have expected us.” – Majibu ya Anonymous kwa mtandao wa HackRead
Ingawa oparesheni hiyo ilihusisha pia udukuzi wa tovuti na mitandao mbalimbali inayomilikiwa na serikali katika nchi za Afrika bado hawakusema kwa moja kwa moja ni kipengele gani katika oparesheni yao kimewafanya hasa washambulie shirika la TTCL.
Jambo jingine ambalo halijaweza kufahamika mara moja ni kama data hizo zinajumuhisha wafanyakazi waliokwisha staafu au kuondoka kwenye shirika hilo.
Mitandao mingine iliyopata kudukuliwa katika oparesheni hii ni pamoja na mtandao wa ajira wa Afrika Kusini na mitandao kadhaa ya serikali za Uganda na Rwanda.
Tumewaandikia barua pepe TTCL kupata taarifa kutoka kwao juu hili jambo na bado hatujapata majibu.
Vyanzo: Twitter, HackRead, na mitandao mbalimbali
2 Comments