Twitter kuwa X. Mmiliki wa app ya Twitter na mfanyabiashara maarufu, Bwana Elon Musk alitangaza na tayari hatua zimeanza kuchukuliwa za kuifanya app ya Twitter kuwa app ya kila kitu (super app), zaidi tuu ya mtandao wa kijamii, na inahusisha kubadili jina la kampuni kwenda X.
Tayari picha zimesambaa kuonesha mabadiliko yakifanyika katika ofisi kuu za kampuni hiyo, kuondoa mabango ya jina Twitter na kuweka lile la X. Pia tayari kwenye toleo la Twitter la kwenye kompyuta logo rasmi kwa sasa ni ya X, huku kwa watumiaji wa app wategemee mabadiliko hayo kuja muda wowote kuanzia sasa.
Elon Musk anaamini kuwa kwa kupitia X anaweza kuleta mageuzi makubwa ya maana ya mtandao wa kijamii na jinsi watu wanaweza kutumia huduma za kifedha wakiwa moja kwa moja ndani ya mitandao ya kijamii – akitaka kuiga mafanikio ya mtandao wa kijamii wa weChat wa nchini China.
Baadhi ya mambo ambayo Elon anataka watu waweze kuyafanya wakiwa ndani ya huduma ya X ni pamoja na uwezo wa kutumiana pesa, na ata kulipia huduma zingine za mbalimbali (kuwa na duka la huduma mbalimbali muhimu duniani kote).
Bado hatuna uhakika kama Musk ataweza kufikia malengo yake ya makubwa kwa kampuni ya X. Hata hivyo, hakuna shaka kwamba yeye ni mjasiriamali ambaye amekuja kufanikiwa kwenye mambo ambayo wengi mwanzoni waliyaona hayawezekani – hii ni pamoja na mafanikio ya Space X, Tesla na Starlink.
Hata hivyo, pia kuna changamoto ambazo X itabidi kukutana nazo:
- Ushindani: Tayari kuna idadi ya app kubwa kwenye soko, uzuri ni kwamba app ya WeChat haijapata mafanikio makubwa duniani kote kama nchini China. Hivyo X ina nafasi, lakini pia tukumbuke bado kuna huduma nyingi zingine ambazo tayari zina apps zake na watumiaji wamezizoea – huduma ambazo Elon anataka watu wazipate wakiwa ndani ya app ya X.
- Udhibiti: Serikali kote ulimwenguni zinazidi kuchukua hatua za kudhibiti sekta ya teknolojia. X inaweza kukabiliwa na changamoto kutoka kwa wasimamizi.
Je kwa mtazamo wako, unadhani kuna nafasi ya app ya X kusimama na kuwa kubwa zaidi? Lengo la kuwa app ya kila kitu – au mambo mengi, lilishajalibiwa na Facebook ila bado halijafikiwa, labda mawazo ya kiutofauti ya Bwana Elon Musk yatafanikisha hili. Ni muda tuu ndio utakaotuonesha picha kamili.
No Comment! Be the first one.