Kampuni ya Uber Technologies italazimika kulipa fidia ya dola za kimarekani milioni kumi ili kusuluhisha kesi iliyofunguliwa dhidi yake baada ya kudanganya juu ya utaratibu unaotumikia kuwachunguza watu ambao wanakuwa madereva wake.
Miji ya San fransisco pamoja na Los Angeles ilifungua kesi ya kiraia ya madai juu ya kampuni hiyo kwamba inatoa kauli zinazopotosha watumiaji wa usafiri huo, hii ilitokana na Uber Technologies kutangaza kwamba utaratibu wake wa kuwachunguza madereva ndiyo utaratibu bora zaidi katika sekta ya usafiri ingawa katika ki uhalisia hawafanyi hayo.
Kwa kawaida watoa huduma za usafiri wa taxi katika miji hiyo huwachunguza madereva juu ya historia za uhalifu wa nyuma kwa kuchukua alama zao za vidole, hata hivyo Uber hawakufanya na hii ilipelekea kuweka mwanya kwa watu ambao walikuwa na historia ya makosa ya jinai kipindi cha nyuma kupata kazi ya udereva katika magari hayo.
Imeamuliwa kwamba Uber walipe kiasi cha dola za kimarekani milioni 10 ndani ya siku 60 na iwapo watashindwa kulipa kiasi hiki katika siku hizo zilizotajwa basi watapigwa faini kubwa zaidi ya dola za kimarekani milioni 15.
Maamuzi hayo ya mahakama yanaenda mbali na kuzigusa biashara zote hasa startups kwamba ni lazima mtu ufute utaratibu na sio kudanganya watumiaji ili tu kupata wateja wengi. Kwa Afrika mashariki kwa mfano ambako zipo biashara nyingi zinaanzishwa ni vyema kwa wamiliki kujifunza kutoka kwa kilichowapata Uber kwa kufuata sheria zilizowekwa ili wasije kuingia hasara baadaye.
Soma zaidi:Uber Kuja Tanzania.
Uber ni kampuni ya usafirishaji ambayo inamruhusu mteja kwa kutumia App kujua madereva walio karibu yake na pia inamruhusu mteja kujua gharama ya usafiri kabla hata ya kumuona dereva. Huduma hii inasemekana kuwa itakuja pia Tanzania baada ya kuwepo katika miji 7 Afrika.
Makala hii imeandikwa kwa msaada kutoka Mtandao wa VERGE pamoja na vyanzo vingine