Je umeshasikia kuhusu Tecno Boom J7? Kwa kiasi kikubwa utakuwa tayari ushasikia kwani kuanzia mwezi wa nne mwaka huu tokea simu hii iingie sokoni kampuni ya Tecno inajitahidi kuitangaza sana. Je ina sifa gani hasa? Endelea kusoma.
Kama unatufuatilia katika akaunti yetu ya Instagram basi utakuwa umeona takribani wiki moja na siku kadhaa zilizopita tuliweka picha ya boksi likiwa na simu hiyo mpya tukikwambia kuwa kaa tayari kuifahamu kwa undani hivi karibuni. Baada ya kuitumia kwa zaidi ya wiki moja sasa naweza kuandika kuhusu simu hii.
Unaweza kuangalia video ya uchambuzi wetu hapa au kupitia akaunti yetu ya YouTube!
Je hii ni simu kwa ajili ya kina nani?
Kwa mtazamo wangu hii ni simu nzuri kwa watumiaji wa aina zote, yaani inagusa wale wanaopenda kumiliki simu janja yenye muonekano na sifa nzuri na huku wakiwa hawapo tayari kutumia pesa nyingi sana katika kupata simu ya aina hiyo.
Kama siku haiwezi kupita bila muziki basi hakika hii ni kwa ajili yako. Ungependa kumiliki hiki chombo? #ItsBoomTime
Posted by Tecno Mobile Tanzania on Friday, April 17, 2015
Pia simu hii inawafaa pia wapenda muziki. Simu hii inayopatikana ikiwa kwenye boksi lenye karibia kila kitu utakachoitaji baada ya kununua simu mpya utakutana na spika za skio ndogo (earphones). Nje ya earphones ndani ya boksi ilo utakuta makava mawili ya rangi tofauti kwa ajili ya simu yako na hivyo kuondoa ulazima wa wewe kwenda kutafuta zingine. Kwa kiasi kikubwa naweza kusema wengi wanatakiwa wafuate mfano huu katika kuuza simu.
Muonekano
> Sio nzito sana na inatosha vizuri kwenye kiganjani. Kwa kipimo ni milimita 143 kwa 71.9, ikiwa na wembamba wa milimita 8.93. Inapatikana katika rangi tatu; Nyeupe, Nyeusi pamoja na rangi ya bati(silver). Jumba lake ni la plastiki.
>Pia simu hii inamanjonjo ya kipekee kama vile uwezo wa kuiamsha pale ambapo imekaa muda mrefu bila kutumika kwa kugusa mara mbili kioo chake.
>Pia ujanja mwingine ni kwamba si lazima uifungue kabisa, yaani kuunlock kama nia yako ni kuchungulia tuu... kuchungulia, gusa kioo chake na kisha kisogeze tuu kuelekea pande yeyote unayotaka kuona. >Pia utaweza kufungua apps kama vile kamera kwa kuandika C kwenye kioo ikiwa kimejipumzisha/kimezima (sleep) na simu ikakupeleka moja kwa moja kwa app husika. Pia unaweza andika W kwa ajili ya Whatsapp, na M kwa ajili ya kufungua app ya muziki. Kama unatufuata kwenye akaunti yetu ya WhatsApp basi utakuwa ushaona haya. ( Bofya – @teknokona Instagram)
Moja ya kitu nilichokipenda katika simu ya #Tecno #BoomJ7 ni uwezo wa kutumia kioo chake kama ‘shortcut’ ya kwenda moja kwa moja kwenye app flani. Hapa ni mfano wa kwenda haraka zaidi kwenye #Whatsapp….angalia video zilizopita kwa maujanja mengine ya simu hii. #TeknoKonaDotCom #Tanzania A video posted by WWW.TEKNOKONA.COM (@teknokona) on
Sifa za Kiundani
> Programu Endeshaji (Android), Simu hii inakuja na toleo la Android 4.4.2 KitKat
>Diski Uhifadhi (Memory Disk), Tecno Boom 7 inakuja na diski uhifadhi wa kiasi cha GB 16, juu ya hili utaweza pia kutumia memori kadi ya ukubwa wa hadi GB 32.
> Inakuja na kiwango cha RAM cha GB 1, hichi ni kiwango kizuri tuu na ukilinganisha na bei ya simu utagundua ni bonge la dili!
>Laini Mbili, inakuja na uwezo wa kutumia laini mbili. Laini moja ni za ukubwa mdogo (Micro Sim) kama zile zinazotumika katika iPhone na ata simu zingine za kisasa zaidi wakati eneo jingine ni la laini ya ukubwa tuliouzoea katika simu nyingi za kawaida.
>Kamera – Kwenye kamera ina megapixel 8 na katika utumiaji wangu naweza nikasema inakiwango kizuri tuu katika eneo hilo. Pamoja na kamera hii kuna teknolojia za HDR, ‘autofocus’ na uwezo wa kupiga picha za Panorama. Pia kuna flash kwa ajili ya uwezo wa kupiga picha kwenye eneo la giza. Inauwezo wa kurekodi video katika kiwango cha pixels 1080 (@30fps).
Kamera ya selfi inakuja na uwezo wa kawaida wa MegaPixels 2. Hii inamaanisha utaweza kupiga picha za selfi ila ni kwa ubora wa kawaida.
>Kiwango cha Betri; Inakuja na kiwango cha betri cha 2020mAh, katika siku zaidi ya 8 ambazo nimekuwa nikiitumia simu hii mara nyingi nimejikuta nikichaji mara moja tuu kwa siku. Ila kama kawaida suala la kuisha chaji linahusiana na jinsi gani unaitumia simu yako.
Teknolojia zingine zinazopatikana katika simu hiyo ni pamoja na redio ya FM, uwezo wa kucheza video na nyimbo za aina mbalimbali.
BEI?
Simu hii inapatikana kwa bei ya Tsh 250,000/=, kutegemea na ulipo nadhani inaweza ikawa ikawa juu kidogo au chini kulingana na utakapoinunua. Ukilinganisha na sifa na kiwango cha simu hii naweza kusema bei hii inaifanya simu hii iweze kuleta ushindani mkubwa kwa simu kutoka kwa makampuni mengine ambazo zipo katika bei ya kuanzia laki tatu.
Ushauri wetu?
- Kama unafikiria kununua simu janja yako ya kwanza yenye kiwango kizuri hautakuwa umepoteza pesa kama ukiamua kununua simu hii.
- Pia kama unafikiria kumnunulia mtu zawadi ya simu, basi simu hii kuanzia kwenye jinsi ya ‘packaging’ yake itakuwa ni zawadi nzuri katika bei inayoeleweka.
- Na pia kama wewe ni mtumiaji wa simu mbili na unafikiria kununua simu ya pili isiyo ghari sana ila pia ikiwa na ubora mzuri basi Tecno Boom J7 litakuwa ni chaguo sahihi
- Uwezo wa laini mbili nao ni faida kwa wale wote ambao hawapendi kutembea na simu mbili ila pia wanapenda kumiliki simu janja ya kiwango kizuri.
One Comment