Uhalifu wa mtandao ni uhalifu unaoshika kasi duniani katika miaka ya karibuni. Hii imetokana na ukuaji wa teknolojia ambapo mambo mengi yamerahisishwa kiutendaji.
Kukua kwa teknolojia, kumetoa pia nafasi kwa wahalifu kubuni mbinu mpya kila wakati ili kufanikisha matukio ya kiuhalifu. Takwimu zinaonesha kuwa kwa kipindi cha Januari hadi Juni mwaka 2017, kumeripotiwa makosa ya mtandao 3,346 nchini, huku wilaya ya Kinondoni ikiongoza kwa kuwa na makosa 1,383.

Mpaka mwishoni wa mwezi Novemba zaidi ya makosa ya mtandaoni 7,900 yaliripotiwa. Mwaka 2016, zaidi ya makosa 8,700 yaliripotiwa huku zaidi ya makosa 7,700 yakipelekwa mahakamani.
Makosa ya mtadao yanajumisha:-
kusambaza taarifa za uongo, kuingilia mawasiliano ya mtu bila ridhaa yake, kusambaza na kumiliki picha za ngono za watoto, kusambaza picha za utupu, uchochezi, kuzidisha muda wa kubakia kwenye mfumo wa kompyuta pamoja na kutuma meseji za uchochezi, n.k.
Kwa sasa asilimia 90 ya makosa yanayofanyika yanahusisha teknolojia ya kompyuta na mawasiliano.
Makosa mengine ni kuzuia upelelezi, kuingilia data kinyume cha sheria, ujasusi wa data, ufichuaji wa taarifa za upelelezi, kughushi kunakohusiana na kompyuta, udanganyifu unaohusiana na kompyuta pamoja na wizi wa haki miliki.
Ni vema kuwa na utaratibu wa kubadilisha namba za siri mara kwa mara ili kuepuka wahalifu kukariri namba yako na kuepuka kutumia namba ya siri moja kwa akaunti zaidi ya moja.