Watu wengi wanahifadhi data zao mtandaoni, kitu amabacho ni bure na kimejipatia umaarufu zaidi hivi karibuni. Hifadhi hii ni kama vile iko hewani, hifadhi-pepe, sehemu ambapo mtu hajui iliko ila anaamini ipo na ipo salama. Unaweza kupata hifadhi hii ya bure, kwenye simu au kompyuta yako.
Kuna kampuni nyingi za hifadhi-pepe ambazo zinatoa huduma kulingana na mahitaji ya mteja ila wengi wanalenga mtumiaji wa kawaida na hutoa huduma hii bure, kwa kiasi kidogo. Kampuni hizo ni kama Dropbox, Box na makampuni kinara ya Microsoft, Google na Apple.
Utajiuliza kwa nini haya makampuni yanakupa hifadhi (Megabaiti, kwa lugha nyepesi) bure?
Teknolojia ya uhifadhi kidigitali imekuwa ya gharama nafuu sana na kampuni hizi zina imani kwamba watu wa kawaida wakizoeshwa kutumia huduma hii ya bure, watu haohao watatamani kulipia kwa huduma zaidi na pia watashawishika kuitumia huduma hii kwenye biashara zao au makampuni wanayofanyia kazi.
Dili tayari zinafanyika kati ya makampuni ya simu na makampuni ya huduma hizi ili kuongezea umaarufu kama siyo utegemezi wa hifadhi-pepe. Dili kama hizi ni kama Dropbox inayokuja na kitumi cha Samsung.
Faida kwa kwako, mtumiaji
Mambo yanavyozidi kwenda kidigitali na watu nao wanabadili jinsi wanavyofanya hayo mambo – kidigitali. Siku hizi, mtu anapendelea zaidi kuhifadhi mafaili yake kwenye hifadhi-pepe ili aweze kuyapata popote alipo.
Unaweza kuweka mafaili ya aina yoyote ambayo si hatarishi kwenye hifadhi pepe. Pia unaweza kucheza muziki, muvi, picha na midia yoyote popote unapotaka.
Hifadhi hii inakurahisishia maisha na kukupa uhuru wa kutobeba vitu pale unaposafiri. Pia, inakuondoa wasiwasi pale unapotaka kupata nyaraka za msingi, pale ambapo haukujitayarisha. Unaweza pia kuwa mtu ambae una vitu vingi vya kushirikisha watu na unahitaji kutuma hivyo vyote kwa wakati mmoja bila kutumia muda mwingi. Mambo yote haya yanasuluhishwa na hifadhi-pepe. Huu ndio uhondo wa teknolojia!
Huduma za hifadhi ya bure ni nyingi na ili unufaike zaidi inabidi uchunguze kidogo nini unachotaka na vipi ambavyo hifadhi hiyo itakupa uwezo zaidi, kwa mfano, Google wanakupa GB 15 za kuhifadhi vitu vyako huku ukiwa na uhuru wa kuitumia pamoja na anuani yako ya barua-pepe, Muvi za Playstore na pia kitumi chako cha Android papo kwa hapo. Pia, unaweza kuandika na kuhariri nyaraka zako popote ulipo hata kama hauna MS Office. Hili ni jambo la faida kwa watu wanaofanya mambo ya kiofisi zaidi na watumiaji wa vitumi vya Android.
Kila kitu kina Kasoro
Kitu kubwa kinachokwamisha hifadhi-pepe ni usalama na faragha. Wataalamu wengi wa masuala ya kidijitali wanatilia shaka matumizi ya hifadhi-pepe, hasa kwa umma ambao wengi hawajui madhara ya kupuuzia faragha. Wiki chache zilizopita mastaa kadhaa walipata shida na hifadhi pepe ya i-cloud pale mahaka walipoingia kwenye akaunti zao na kuiba na kuanza kuzisambaza picha binafsi za mastaa hao mtandaoni.
Pamoja na hayo, watu wengi wanatumia huduma hizo na zinaendelea kuwa na umaarufu sana. Ni muhimu zaidi kujua kwamba, kutumia huduma hizi za bure zinahitaji uamuzi makini wa vitu utakavyoweka. Ni vyema kujiwekea sera ya kwamba kitu chochote nyeti na chochote cha faragha kama picha, sauti na video hakifai kuhifadhiwa mtandaoni kwa namna yoyote hata kama kitu hicho kilitumwa mtandaoni.
Je wewe unatumia hifadhi yako ya bure? Jiunge nasi na watu wengine na utufahamishe kupitia facebook hapa na twitter hapa.
No Comment! Be the first one.