Edward Snowden, mtu mashuhuri kwa kitendo chake cha kuvujisha siri kubwa za uvunjwaji wa sheria na utaratibu unaofanywa na shirika la usalama la Marekani – NSA, amejiunga katika mtandao wa Twitter kwa kishindo.
Tweet yake ya kwanza alitweet kimombo kwa maneno yenye maana karibia na “unaweza nisikia sasa?”, hadi sasa tweet hiyo imeweza kusambazwa (retweets) zaidi ya mara 100,000.
Bwana Snowden alivujisha siri nyingi mwezi wa sita mwaka 2013. Data alizozitoa kwa waandishi wa habari zilionesha kwa kiasi kikubwa jinsi gani shirika la usalama la Marekani (NSA) lilikuwa linatumia njia za panya na teknolojia kubwa katika kuhakikisha wanafahamu mambo mbalimbali yanaendelea katika simu na kompyuta za watu wanaotumia huduma za intaneti nchini Marekani na hadi kwa baadhi ya viongozi wa juu wa mataifa rafiki wa Marekani.
Uvujishaji wa data hizo za siri wa hali ya juu ulimlazimu akimbie nchi hiyo na mwisho wa siku kujikuta akipewa hifadhi nchini Urusi, mbali na mikono ya vyombo vya dola vya Marekani.
Kwa wengine nchini Marekani Bwana Snowden ni shujaa na kwa baadhi anaonekana kama ni msaliti wa taifa hilo.
Dakika chache baada ya kufungua akaunti yake ya kijamii ya Twitter jumanne asubuhi akaunti hiyo iliweza kuwa ‘verified’ na Twitter, alamu ya kuonesha ni akaunti halisi ya Bwana Snowden. Ndani ya lisaa aliweza kupata Followers zaidi ya elfu 70. Sasa hivi akaunti hiyo ishafikisha Followers karibia milioni 1.
Yeye mwenyewe ana’follow akaunti moja tuu, ya shirika la usalama la Marekani, NSA.
Baadhi ya data alizovujisha zilionesha ni kwa namna gani shirika la usalama la Marekani lilikuwa linachungulia data za watu kwenye huduma za barua pepe na mitandao ya kijamii, mitandao mingi imechukua hatua nyingi zaidi kuweza kufanya mitandao yao iwe salama zaidi. Uamuzi wake wa kujiunga mtandao wa Twitter unaonesha pia amekubali hatua za kiusalama wa data zilizochukuliwa na mtandao huu maarufu.
Ukitaka kum’follow Twitter anapatikana kwa @Snowden , pia kumbuka kuungana nasi Twitter kupitia @teknokona
No Comment! Be the first one.