Unafikiri watu wanatumia sana apps za mitandao ya kijamii siku hizi ukilinganisha na mwaka 1, miwili nyuma? Data zinaonesha vinginevyo – utumiaji unashuka katika mitandao yote mikubwa, Facebook, Instagram, Snapchat na Twitter.
Katika data zilizotolewa na kampuni ya ukusanyaji data ya SimilarWeb inaonesha wastani wa muda unaotumika katika apps za mitandao hiyo kwa watumiaji wa simu za Android mwaka huu umeshuka ukilinganisha na kipindi hicho hicho hapo mwaka jana (2015).
Data hizo zilizojikita katika apps za Facebook, Instagram, Snapchat na Twitter pia ziliangalia nchi kadhaa zenye watumiaji wengi – Marekani, Uingereza, Ujerumani, Uispania, Australia, Afrika Kusini, India, na Brazili.
App ya Instagram ndiyo iliyoshuka zaidi katika utumiaji katika app hizo, utumiaji wa Instagram umeshuka kwa takribani asilimia 23.7 mwaka huu. Twitter ikifuatia kwa asilimia 23.4, Snapchat kwa asilimia 15.7 na mwisho Facebook utumiaji ukishuka kwa asilimia 8.
Je kushuka ni kwa kiasi gani?
Ingawa karibia katika nchi zote utumiaji umeshuka ila umetofautiana, mfano utumiaji wa app ya Snapchat nchini Brazili umeshuka kiasi tuu, yaani kutoka dakika 11.23 mwaka jana, hadi dakika 11.10 mwaka huu.
Ukilinganisha na kwa app ya Twitter Ufaransa mwaka jana (Q1) umeshuka sana kutoka dakika 19.80 hadi kufikia dakika 13.12, hili ni poromoko kubwa…takribani asilimia 34.
Utumiaji wa apps za Mitandao ya Kijamii – Data (SimilarWeb)
(Upande wa muda ni katika Dakika)
Ukiachana na kushuka kwa muda ambao watu wanatumia app hizo kwa siku pia ata idadi ya upakuaji (install) wa app hizo umeshuka pia. Mfano upakuaji wa app ya Snapchat nchini Afrika Kusini umeporomoka kwa asilimia 56 katika kipindi hicho (Machi 2015 hadi Machi 2016). Ila kwa ujumla wake apps hizo 4 upakuaji wake umeporomoka kwa asilimia 9 katika nchi hizo zilizohusishwa na utafiti huu.
Vipi wewe una mtazamo gani juu ya data hizi? Je utamiaji wako wa apps gani umeshuka ukilinganisha na mwaka jana?
Chanzo: SimilarWeb