Kila mwaka, Apple hutuletea matoleo mapya ya mfumo wake wa uendeshaji wa iOS, na mwaka huu, iOS 18 inakuja na mambo mengi mapya ambayo pengine yatawafurahisha watumiaji wa iPhone. Huku tukitarajia iOS 18 kuachiliwa rasmi mwezi September,embu tuanglie baadhi ya vipengele vipya ambavyo vinaonekana kuvutia zaidi.
Vipengele Vipya na Vilivyoboreshwa katika iOS 18
1. Apple Music Yenye Akili Mnemba(AI)
Katika iOS 18, Apple Music imepata maboresho makubwa kwa kutumia teknolojia ya AI. Mfumo huu utatengeneza orodha za muziki kulingana na ladha yako ya muziki. Hii inamaanisha huna haja ya kutafuta orodha bora ya nyimbo kwani Apple Music itakufanyia kazi hiyo, sawa na kile Spotify inavyotoa.
2. Uhariri wa Picha Kutumia Akili Mnemba.
Apple sasa imeingiza zana ya kurekebisha picha kwa kutumia AI ndani ya programu ya Photos. Mfumo huu utaweza kugundua na kuondoa vipengele visivyohitajika kama vile watu waliovuruga picha zako au vitu visivyotakiwa kwenye mandhari. Hii itakusaidia kuboresha picha zako za kumbukumbu na kufanya ziwe safi na za kuvutia.
3. Uandishi wa Manukuu ya Sauti
Kwa kutumia iOS 18, programu ya Voice Memos itapata uwezo wa kuandika manukuu ya sauti moja kwa moja wakati wa kurekodi. Hii itakupa fursa ya kuona maandiko ya kile unachorekodi kwenye skrini. Huu ni uboreshaji mkubwa hasa kwa wale wanaopenda kuhifadhi kumbukumbu za sauti.
4. Tap To Cash
Tap To Cash ni kipengele kipya kitakachokuwezesha kutuma na kupokea pesa kwa urahisi kwa kushikilia iPhone yako karibu na ya mtu mwingine. Hakuna haja ya kubadilishana namba za simu. Hii itarahisisha malipo wakati uko na marafiki au familia.
5. Kubadilisha Mandhari ya Skrini.
Katika iOS 18, utakuwa na uwezo wa kubadilisha rangi na mandhari ya skrini ya mwanzo, pamoja na kupanga upya na kubadilisha ukubwa wa ikoni za programu. Hii inamaanisha unaweza kubinafsisha muonekano wa simu yako kwa kiwango kikubwa zaidi.
6. Ujumbe wa Kujipangia Wakati wa Kutuma(scheduling)
Sasa utaweza kupanga kutuma ujumbe kwenye programu kama iMessage, Mail, na SMS kwa muda maalumu. Hii ni njia nzuri ya kuhakikisha hujakosa kutuma ujumbe muhimu. Pia, Notes App imeboreshwa na sasa unaweza kuingiza hesabu yoyote na itahesabiwa papo hapo.
7. Genmoji
Genmoji ni kipengele kipya ambacho kitakuruhusu kuunda emoji zako kwa kutumia maelezo. Hii ni njia mpya ya kufurahisha ya kutumia emoji.
8. Marekebisho ya Siri kwa AI
Siri imeboreshwa na sasa inaweza kuelewa amri zako bila kugusa simu. Unaweza kujibu simu kwa kutikisa kichwa au kuipiga picha kwa kutumia amri za sauti. Hii itawasaidia watumiaji ambao hawana ujuzi wa teknolojia kutumia kamera ya iPhone kwa urahisi zaidi.
iOS 18 imekuja na maboresho mengi ya kuvutia ambayo yanaonyesha dhamira ya Apple ya kuendelea kuboresha uzoefu wa mtumiaji. Ingawa baadhi ya vipengele vinaweza kuwa vimechelewa, tunaamini watumiaji wa iPhone watafurahia maboresho haya na tunasubiri kwa hamu kuona jinsi itakavyofanya kazi katika matumizi halisi.
No Comment! Be the first one.