Kama ulikuwa hauijui Periscope basi ni app inayomilikiwa na Twitter ambayo ni mahususi kwa kurusha video za moja kwa moja (LIVE) za watumiaji wa Twitter.
Periscope ni njia ya Twitter kupambana na mitandao mingine kama vile Snapchat Instagram na Facebook ambayo imejipatia umaarufu kwa video za kurekodi na zile za moja kwa moja.
Periscope wamefanya mabadiliko katika app yao na sasa wataweza kuruhusu video za watumiaji kukaa mda mrefu baada ya mtumiaji kumaliza kuirusha moja kwa moja, mwanzoni video zilikuwa zinaweza kukaa kwa masaa ishirini na nne tu. Hii haikupendwa sana na wafanyabiashara na watu wa matangazo kwakuwa ilikuwa inapunguza muda ambao watumiaji wangeweza kuiona video hivyo kupunguza muda ambao tangazo linaweza kuangaliwa.
Periscope ilitengenezwa ili kusaidia Twitter kuwa na ukuwaji wa watumiaji walio hai, hivyo ilikuwa ni lazima pamoja na mambo yote ifanye yale ambayo watumiaji wanayapenda na ni wazi kwamba watumiaji wanataka kuona video wanazoposti zinakaa muda mrefu zaidi ya masaa 24.
Watumiaji wa mtandao huu hivi sasa watakuwa na uhuru wa kuchagua kama video zao ziendelee kuwepo baada ya masaaa 24 ama zifutike baada ya masaa ishirini na nne, kama utahitaji video zako za periscope ziendelee kuwepo hata baada ya masaa ishirini na nne itabidi uweke #save popote katika jina la video hiyo.
App hii ya Twitter inaweza kutumika kwa mambo mengi ya kimaendeleo na pia kwaajiri ya kujiburudisha na kwaburudisha washkaji, wapo ambao wanatumia periscope kutangaza biashara zao mfano nguo wapo ambao wanatumia app hii kuendeshea shughuri zao za udalali kwa kuweka video za nyumba za wateja wao zinazopangishwa ama kuuzwa. Ni juu yako kama utaitumiaje app hii ya Periscope ili mradi unayo akaunti ya Twitter basi sio kitu kibaya kujaribu.
Twitter ambayo imekuwa katika nyakati ngumu baada ya hisa zake kutokuwa zinafanya vizuri katika soko imekuwa katika jitahada za kila namna za kuongeza watumiaji hai, hii ni karata nyingine ambayo mtandao huu unatupa kwaajiri ya kujaribu kujinusuru na kushindwa vita ya mitandao ya kijamii.
Makala hii imeandikwa kwa msaada wa mtandao wa CNBC na mitandao mingine.