Miwani ya AI ilipaswa kufanya maisha yawe rahisi. Ikuonyeshe unachokiona, ikusaidie kukumbuka, kutafsiri na kujibu maswali bila kutoa simu mfukoni. Lakini kesi inayohusisha Meta imeibua upande mwingine wa teknolojia hiyo. Mawakili wanaowawakilisha watumiaji wanadai wafanyakazi waliokagua data ya Meta walitazama na kuweka alama kwenye video zilizorekodiwa na Ray-Ban zikiwaonyesha watu wakibadilisha nguo, kutumia choo na kushughulikia taarifa za kifedha. Video hizo zilikuwa zimefika kwenye seva za Meta kwa ajili ya kuboresha mifumo ya AI. Meta imekana madai hayo na imesema itayapinga mahakamani.
Tatizo hapo si mtu mmoja kurekodi video. Ni kwamba kamera iliyoko kwenye uso wa mtu mmoja inaweza kukusanya taarifa za watu wengine ambao hawakununua kifaa, hawakukiwasha na huenda hawakujua hata wanarekodiwa.
Kamera Inapokuwa Sehemu Ya AI
Hii ndiyo tofauti ya miwani ya AI na kamera ya kawaida. Kamera ya simu unapoitoa, watu wanaweza kuona unachofanya. Lakini miwani inaweza kukaa usoni wakati wote. Meta inasema Ray-Ban zake zina taa inayoonyesha wakati wa kurekodi na kamera huzimwa ikiwa taa hiyo imefunikwa au kuchezewa. Lakini taa ndogo kwenye fremu ya miwani haimaanishi kila mtu aliye karibu ataiona.
Nchini Uingereza, Wetherspoon imezuia matumizi ya miwani hiyo katika maeneo yake. Nchini Ufaransa, mamlaka zimeanza kuchunguza matumizi ya smart glasses baada ya malalamiko kuhusu kurekodi watu bila ridhaa. Australia nayo inatafakari kuzuia miwani yenye kamera kwenye maeneo ya serikali kwa sababu ya faragha na usalama.
Hii inaonyesha kwamba mjadala hauko tena kwenye “je, watu watazipenda smart glasses?” Unaanza kuwa kuhusu watu wengine watakubali kuishi karibu na kamera hizo?
Kampuni Zinaanza Kutafuta Njia Nyingine
Baadhi ya kampuni zimeamua kuondoa kamera kabisa. Even Realities ilianza kuuza miwani yake ya G1 bila kamera mwaka 2024. Kampuni hiyo imeeleza kuwa watu wameanza kuhusisha smart glasses na kurekodiwa kwa siri, hivyo kamera zinapaswa kusubiri hadi kuwe na ulinzi madhubuti zaidi.
Pocket imechagua kifaa kinachowekwa kwenye simu na kinahitaji mtumiaji kubonyeza kitufe ili kurekodi. Plaud nayo ina virekodi vya AI vinavyowashwa na mtumiaji na kutoa ishara kwa watu walio karibu.
Kuna tofauti kubwa hapa: kampuni hizi zinajaribu kufanya kurekodi kuwe kitendo cha makusudi, badala ya kitu kinachoweza kutokea wakati wote.
Hata OpenAI Inaona Tatizo Hili
Sam Altman amewahi kueleza maono ya kifaa cha AI kinachoweza kuelewa mazingira ya mtumiaji muda wote, lakini alisema aina hiyo ya kifaa itahitaji kuchakata data nyingi ndani yake badala ya kutuma kila kitu kwenye cloud. Sababu ni rahisi. Kifaa kinachotazama na kusikiliza maisha yako muda wote kinaweza kuwa na taarifa nyingi sana za kibinafsi. Altman alisema watu wengi hawatataka maisha yao yote yaendelee kutumwa kwenye seva za kampuni.
Hapo ndipo sekta nzima inakutana na tatizo moja. AI inakuwa na manufaa zaidi inapojua zaidi kuhusu mazingira yako. Lakini kadiri inavyojua zaidi, ndivyo inavyoweza kujua kuhusu watu ambao hawakuchagua kushirikishwa.
Na Hili Linamhusu Pia Mtanzania
Tanzania bado haijafikia kiwango ambacho smart glasses ni sehemu ya maisha ya kila siku. Lakini teknolojia haiji ikiwa imekamilika kwanza halafu ndipo inafika kwetu. Simu zetu tayari zina kamera, maikrofoni, location, assistants na AI zinazoweza kuelewa picha, sauti na mazingira. Vifaa vinavyovaliwa vinaendelea kuongeza uwezo huo.
Sasa fikiria mkutano wa biashara, hospitali, ofisi, darasa au sehemu ya starehe ambapo mtu mmoja amevaa kifaa kinachoweza kurekodi na kuchambua mazingira yake. Mtu huyo amekubali. Je, watu wengine waliomo humo wamekubali pia?
Hilo ndilo swali ambalo sheria za faragha zitahitaji kulikabili kadiri vifaa hivi vinavyoenea. Kwa sababu data inayokusanywa na kifaa cha AI si lazima iwe ya mtu aliyekinunua.
Simu Ilitupitisha Hapa. AI Inatupeleka Wapi?
Tulipoanza kutumia simu zenye kamera, watu walihofia pia kurekodiwa kila mahali. Baadaye tukazoea. Smart glasses zinaweza kupitia mchakato huo huo. Lakini kuna tofauti moja kubwa: kamera sasa iko kwenye uso wa mtu na inaweza kuwa sehemu ya maisha yake muda wote. Hapo ndipo biashara hii inaweza kukutana na kizuizi chake kikubwa. Si kamera. Si AI. Si betri.
Ni imani ya watu kwamba kifaa kilicho karibu nao hakitawafanya waishi kama kila dakika inaweza kurekodiwa. Na kama kampuni zitashindwa kujenga imani hiyo, huenda tatizo la smart glasses lisikuwa teknolojia kushindwa kufanya kazi. Huenda likawa teknolojia kufanya kazi vizuri sana.
👇 Ukiwa kwenye sehemu ya kawaida na mtu aliye karibu yako amevaa miwani ya AI, ungejisikia salama kujua kwamba inaweza kuwa inarekodi mazingira yenu?
Soma Pia:
Mfululizo wa Matukio Yenye Wasiwasi na Siku Kumi Zilizobadilisha AI
Kwa Nini AI Inaweza Kufanya Simu na Laptop Zako Kuwa Ghali Zaidi?
Vyanzo:
Reuters — From smart glasses to AI pins, privacy fears challenge tech’s next big bet
Reuters — French prosecutors and regulators step up scrutiny on smart glasses
Reuters — Australia considers banning the use of smart glasses in government buildings
No Comment! Be the first one.