Mwaliko wa kujiunga kwenye mradi wa sera za AI unaweza kuonekana kama fursa nzuri kwa mtafiti. Lakini kwa baadhi ya wachambuzi nchini Marekani, mwaliko huo ulikuwa mtego. Kundi la wadukuzi linalofuatiliwa kama TA419 lilijifanya wataalamu wa AI na maafisa wa zamani wa serikali ya Marekani, likawasiliana na wataalamu wa sera za AI na kuwaalika kwenye miradi ya utafiti na ushauri. Lengo lilikuwa kuwafanya waamini mtu waliyekuwa wakiwasiliana naye, kabla ya kuwatumia viungo vilivyolenga kuiba taarifa za kuingia kwenye akaunti zao.
Mtego Ulianza Kwa Jina Linaloaminika
Kuanzia Julai 2026, TA419 ilijifanya watu wakiwemo Lynne Parker, aliyewahi kuwa katika White House Office of Science and Technology Policy, na Heidi Crebo-Rediker, mtaalamu wa uchumi na sera za nje. Walengwa waliombwa kujiunga na kamati bandia ya ushauri kuhusu AI au kuchangia ripoti kuhusu udhibiti wa AI, usafirishaji wa teknolojia na supply chains. Baada ya mlengwa kujibu, wadukuzi walituma kiungo kilichoonekana kama nyaraka za kushirikiana, lakini mwishowe kilimpeleka kwenye ukurasa bandia wa OneDrive uliolenga kunasa credentials za Microsoft.
Mmoja wa waliolengwa alikuwa Alex Engler, mkuu wa Penn Center on Media, Technology, and Democracy. Ujumbe alioupokea ulionekana umetumwa na Parker. Engler alipoutilia shaka na kuthibitisha taarifa hiyo kupitia watu wengine katika sekta hiyo, aligundua kuwa mtumaji hakuwa mtu aliyedaiwa kuwa. Proofpoint ilisema kampeni hiyo iliwalenga watu wachache, chini ya 10 katika taasisi kadhaa za Marekani.
Kwa Nini Wachambuzi wa Sera za AI?
Walengwa hawakuwa wataalamu wa kawaida wa teknolojia. Walikuwa watu wanaofanya kazi kwenye sera za AI, udhibiti wa teknolojia, export controls na mikakati ya kitaifa. Proofpoint inatathmini kuwa kampeni hiyo huenda ililenga kupata taarifa kuhusu mwelekeo wa sera na udhibiti wa AI nchini Marekani, wakati Washington na Beijing zikishindana kuhusu teknolojia hiyo.
Hata hivyo, kuna tofauti muhimu kati ya tathmini na ushahidi. Proofpoint inaihusisha TA419 na China, lakini Reuters haikupata ushahidi wa moja kwa moja kwamba serikali ya China iliagiza operesheni hiyo. Beijing imekuwa ikikanusha madai ya kuendesha ujasusi wa mtandaoni.
AI Sasa Imekuwa Taarifa ya Kimkakati
Kinachofanya kampeni hii kuwa muhimu si tu kwamba wadukuzi walijaribu kuiba nywila. Walichagua watu wanaohusika na maamuzi kuhusu mustakabali wa AI Marekani. Serikali zinaweka sheria za AI, zinaamua vikwazo vya usafirishaji wa chips na teknolojia, huku kampuni zikishindana kujenga mifumo yenye nguvu zaidi. Taarifa kuhusu mwelekeo wa sera hizo zinaweza kuwa muhimu kwa yeyote anayefuatilia ushindani huo.
TA419 pia imewahi kulenga watu katika sekta za ulinzi, usalama wa taifa, nishati na sera za kimataifa. Kampeni hii inaonyesha jinsi taarifa kuhusu AI yenyewe zinavyozidi kuwa sehemu ya ushindani wa kimkakati: wakati kampuni zikishindana kujenga mifumo bora, watu wanaojadili sheria, usalama na mipaka ya teknolojia hiyo nao wanaweza kuwa walengwa.
Na mtego haukuanza kwa programu hatari au faili linaloshukiwa. Ulianza kwa jina la mtu halisi, mada ambayo mlengwa anaifahamu na mwaliko ambao ungeweza kuonekana kama fursa ya kawaida ya kikazi. Hapo ndipo phishing ya kisasa inakuwa ngumu kuitambua: si lazima mshambuliaji akuombe nywila kwenye ujumbe wa kwanza. Anaweza kwanza kukufanya uamini unazungumza na mtu sahihi.
Wezesha bando kwa kutuma kiasi chochote kupitia Selcom, kwenye simu yako bofya *150*50*1# kwenye namba ya malipo weka 60751369 jina litakuja TEKNOKONA.
No Comment! Be the first one.