Je unatumia Snapchat au Telegram na unataka kuweka link ya kuwapeleka watu kwenye akaunti yako hiyo kupitia huduma ya WhatsApp au Instagram? Haiwezekani tena.
Kama adui ananenepa kupitia kula kwako utafanyaje? Mpige marufuku? Inaonekana ndio uamuzi uliochukuliwa na Instagram na WhatsApp dhidi ya link za Telegram
Katika hatua inayoonekana ni kuzuia ukuaji wa huduma shindani huduma ya WhatsApp na sasa Instagram pia ambazo zote zipo chini ya kampuni ya Facebook zimezuia watu kurusha au kuweka link za huduma shindani za SnapChat na Telegram.
Kivipi?
Kwenye WhatsApp ingawa unaweza kuweka link mbalimbali na link hizo zikaweza kubonyezeka ila ukiweka na kutuma kwa mtu ujumbe wenye link inayompeleka mtu kwenye huduma ya Telegram link hiyo haitapokelewa kama link. Inapoteza uwezo wa kuwa link na hivyo kuwa kama ujumbe tuu.
Kwa sasa ni watumiaji wa WhatsApp toleo la Android tuu ndio haiwezekani kutuma links za Telegram, inaonekana ni jambo gumu bado kulizuia katika iOS kwa simu za iPhone. Ila watumiaji wa WhatsApp wa Android ni asilimia 80 ya watumiaji wote.
Telegram wakilalamika na kuonesha ukiritimba wa Facebook
Another @Facebook tentacle closes on users’ ability to share a link to their Telegram profile. #hypocrisy pic.twitter.com/xC6ydp3M0p
— Telegram Messenger (@telegram) March 2, 2016
Kwenye Instagram watu wengi wamekuwa wakiweka link zao hasa za huduma kama vile Snapchat au Telegram…huku wakiwaambia marafiki wawa-follow/Add kwenye huduma hizo pia. Kuanzia sasa ukiandika link kama ni za Snapchat au Telegram zitakataliwa.
Je ni hofu dhidi ya ushindani?
Kwa kiasi kikubwa wengi wameona suala hilo ni kupunguza kasi ya ukuaji wa Snapchat na Telegram…..hasa hasa ikiwa inaonekana dhahiri huduma hizo zinakua zaidi kupitia watu kuambiana kwa kutumia huduma za WhatsApp na Instagram.
Huduma ya kuchati ya Telegram imezidi kukua na sasa imefikisha wastani wa zaidi ya takribani watumiaji milioni 100 kila mwezi na ikiwa na sifa/uwezo kemukemu zikilinganishwa na zile zinaopatikana katika WhatsApp – Soma makala yetu Je ni App gani ni Zaidi kati ya WhatsApp na Telegram ktk kuchati
Kwa kiasi kikubwa haileti maana kuona ni huduma hizo tuu ndio zimezuiliwa, huku huduma nyingine zenye mabavu ya kulipizia zikiachiwa – kama vile YouTube, Twitter, LinkedIn n.k. Yote ni mitandao ya kijamii, ila inaonekana hiyo haijaathirika zaidi kwa kuwa haishindani moja kwa moja na huduma za WhatsApp na Instagram.
Je ni uamuzi ulio sahihi?
Ingawa uamuzi huu unaonekana ni wa kujilinda zaidi kwa WhatsApp na Instagram inaonekana muda si mrefu unaweza ukaingiza kampuni ya Facebook (wamiliki wa WhatsApp na Instagram) matatani. Sheria dhidi ya uhuru katika ushindani katika bara la Ulaya na ata Marekani ni kali sana na inaonekana muda si mrefu kesi dhidi ya WhatsApp na Instagram zinaweza funguliwa. Watumiaji mbalimbali wa Instagram wameshaanza kuponda uamuzi huo.
Soma Pia – Fahamu nani zaidi kati ya app za WhatsApp na Telegram