WileyFox ni kampuni mpya inayojishughulisha na utengenezaji na uuzaji wa simu janja nchini Uingereza.
Mwaka jana kampuni ijulikanayo kama WileyFox ilizindua simu janja zinazotengenenezwa na kampuni hiyo. Kampuni hiyo ni mpya yenye makao makuu yake nchini Uingereza. Uingereza sio maarufu kwa utengenezaji wa simu janja lakini WileyFox wameonekana kutaka kufanya wajulikane ndani na nje ya Uingereza kwa utengenezaji wa simu janja.
Mwaka jana kampuni hiyo ilizindua matoleo mawili ya simu janja: WileyFox Swift na WileyFox Storm kati ya mwezi Septemba na Oktoba mwaka jana.
WileyFox Swift ina kamera yenye 13 megapixels, 5 megapixels kwa kamera ya mbele na pia inatumia simcard mbili, betri yake inaweza kutoka, ina sehemu ya kuweka SD card. Inauzwa £129 (Takribani Tsh 370,000/=).
Huku WileyFox Storm ikiwa na kamera yenye 20 megapixels, 8 megapixels kwa kamera ya mbele(selfie) na kioo chenye urefu wa inchi 5.5 na inauzwa £199 (Tsh 570,000/=).
Simu janja hizo zinatumia toleo spesheli la programu endeshaji ya Andoid ya familia ya Cyanogen.
Mmiliki wa kampuni hiyo Bw. Nick Muir amesema kuwa kampuni yake haitegemei kupata hasara kutokana na Uingereza kujitoa EU kwani wao tayari wana soko China na kwingineko na bidhaa zao zinaaminika na kupendwa ndani na nje ya Uingereza. Pia wana mpango wa kutanua biashara yao nchini Italia, Ufaransa, Ujerumani na Hispania.
Kama makampuni mengine yanayokuwa kwa kasi ya nchini China, kampuni hii inategemea kuuza simu zake kupitia njia ya mtandao tuu. Hii inasaidia kupunguza gharama mbalimbali na hivyo kuhakikisha simu zao zinakuwa za bei nafuu zaidi.
Tangu kampuni hiyo ianze kutengeneza simu janja imetengeneza simu janja zaidi ya laki mbili na nusu na kuziuza kupitia Amazon na kampuni hiyo imetoa toleo lake la tatu Juni 28 mwaka jana ambapo simu janja hiyo ina maboresho mengi na inauzwa £200 (Tsh 373,000/=). Wao kama kampuni watatanua wigo wa biashara na kuanza kuuza simu zao Mashariki ya Kati pamoja na Afrika.
Je, una la ziada ungependa Teknokona tukufahamishe kuhusiana na simu janja hii kutoka Uingereza? Tuambie katika comment nasi tutashughulikia maoni yako/swali lako.
Chanzo: The Teelgraph, AndroidCentral