Data zinazoonesha hali ya utumiaji wa programu endeshaji (OS) kwenye kompyuta duniani kote unaonesha programu endeshaji ya Windows 10 inatumika kwenye zaidi ya Asilimia 14 ya kompyuta zinazotumika kwa sasa.
Shirika la NetMarketShare linaloaminika sana katika utoaji wa takwimu na data zinazohusu utumiaji wa huduma za kimitandao na teknolojia kwa ujumla unaonesha kufikia mwezi wa nne mwaka toleo la Windows 10 limefanikiwa kushika nafasi ya pili kama programu endeshaji iliyokwenye kompyuta nyingi zaidi.
Namba moja bado ni Windows 7 ikiwa na asilimia 48.79, huku Windows 10 ikiwa na asilimia 14.35. Ukuaji wa Windows 10 unaonekana kuathiri zaidi Windows XP na Windows 7.
Data za mwezi wa tatu zilionesha Windows 7 ilikuwa kwenye asilimia 51.89, na kwa mwezi wa nne asilimia hizo zimeshuka hadi kufikia 48.79.
Data kutoka Microsoft za mwishoni wa mwezi wa tatu zilisema programu endeshaji hiyo tayari ipo katika vifaa zaidi ya milioni 270 – ingawa data zao hazikuonesha tofauti ya idadi kwa kompyuta na simu zao zinazotumia Windows 10.
Data hizo zinaonesha utumiaji wa programu endeshaji zingine kama vile za Linux bado upo mdogo. Ata programu endeshaji ya Mac OS X inayotumika katika kompyuta za Apple (Mac & MacBooks) bado ni mdogo pale ukilinganisha na za familia ya Windows.