Kufikia mwishoni mwa mwaka 2015 data kutoka shirika la Net Applications linaonesha hadi sasa ni takribani kompyuta milioni 164 zinatumia programu endeshaji ya Windows 10.
Programu endeshaji hii mpya kutoka Microsoft ni moja ya programu endeshaji zilizotangazwa zaidi na kusifiwa zaidi kama moja ya maboresho bora zaidi kutoka Microsoft katika eneo la programu endeshaji.
Kiasilimia hii inamaanisha kufikia mwishoni mwa mwezi wa 12, 2015 Windows 10 inachangia asilimia 10.7 ya programu endeshaji zote zinazotumika, hii ni asilimia moja zaidi ukilinganisha na data za mwezi wa 11.
Kwa kiasi kikubwa inaonekana kasi ya kupata watumiaji wapya imeshuka sana, hili ni jambo la kawaida na linalotegemewa katika eneo hili. Ila kwa kiasi flani asilimia ya watumiaji bado ni ndogo miezi 5 tokea programu endeshaji hii itoke ukilinganisha na mafanikio ya programu endeshaji ya Windows 7 katika kipindi cha muda huo huo.
Programu endeshaji ya Windows kutoka Microsoft inakisiwa kutumika kwa takribani asilimia 91.3 ya kompyuta zote – asilimia zingine zikishikiliwa na MacOS kutoka Apple na programu endeshaji za Linux (Ubuntu, Fedora, n.k).
Wengi walitegemea kasi ya utumiaji wa Windows 10 ingekuwa kwa kasi zaidi kwa sababu programu endeshaji hii ni ya kwanza kutoka kwa Microsoft kuweza kupatikana bure kwa watumiaji wengi. Kufikia mwezi Oktoba takribani kompyuta milioni 110 zilikuwa zinatumia programu endeshaji hii na hivyo kumekuwa na ongezeko la kompyuta milioni 54.
Windows 7 ilifanikiwa kushikilia asilimia 11.9 katika kipindi chake cha miezi mitano ya mwanzo, Windows 10 imefikisha asilimia 10.7. Tofauti ni ndogo ila ni muhimu kukumbuka ya kwamba Windows 10 inapatikana bure kwa watumiaji wengi wa Windows 7, na inasemekana bado wengi wameamua kutosasisha programu endeshaji zao kwenda Windows 10. Kwa kiasi flani mafanikio katika kiwango cha uwekwaji kwenye kompyuta bado haujafikia kiwango cha kuridhisha zaidi ila bado kuna ukuaji endelevu.
Je umeshakwisha tumia toleo la Windows 10? Tuambie umependezwa na nini zaidi? Kwa habari zaidi na uchambuzi wa toleo la Windows 10 bofya hapa -> TeknoKona – Windows 10
Soma uchambuzi wa Windows 10 hapa-> http://teknokona.com/2014/09/30/microsoft-waruka-windows-9-na-kuja-na-windows-10/
Usipitwe na habari, jiunge nasi katika mitandao ya kijamii – Facebook, Twitter, na Instagram
Vyanzo: Google News, Computer World & Net Applications
No Comment! Be the first one.