Afisa wa kampuni ya Microsoft atoa rasmi data za ukuaji wa utumiaji wa programu endeshaji ya Windows 10 hadi sasa, idadi ya watumiaji imefikia milioni 200.
Kuna sababu nyingi za wao kuamua kutoa data hizi ila kwa kiasi kikubwa wametaka kuonesha ni kwa jinsi gani wanapata mafanikio mazuri katika utumiaji wa Windows 10 hadi sasa. Na pia imekuwa muhimu wao kutoa data rasmi baada ya wengi kutoa makadirio ambayo yanaonesha ukuaji mdogo kuliko uliotegemewa.
Idadi hii vifaa milioni 200 inakuwa imefikia 1/5 ya lengo la Microsoft ya kuifanya programu endeshaji ya Windows 10 kutumiwa katika vifaa bilioni moja duniani kote.
Ukuaji huu wa utumiaji umeifanya Windows 10 pia kuwa programu endeshaji yao ambao usambaaji na utumiaji wake umekua kwa kasi zaidi ukilinganisha na matoleo yaliyopita, yaani Windows 8, 7, Vista n.k. Lakini ni muhimu kujua ya kwamba zaidi ya asilimia 40% kutoka kwenye idadi hii ya vifaa milioni 200 ni vifaa ambavyo vimeanza kutumika baada ya kipindi cha mauzo makubwa ya pungufu ya bei na ofa mbalimbali ya nchini Marekani katika siku inayofahamika kama Black Friday. Hii inamaanisha wengi walijinunulia au kununulia wengine zawadi vifaa mbalimbali vilivyokuja moja kwa moja na Windows 10 ndani yake – hii inaweza ikawa ni kompyuta, tableti n.k.
Lakini pia katika taarifa yao Microsoft pia wamelaumiwa kwa kuonesha ni kwa namna gani toleo la Windows 10 linasoma tabia za utumiaji wa kompyuta za watu na ripoti hiyo kutumwa kwa Microsoft. Kwani wamedai pia kwenye mwezi wa kumi na mbili tuu watumiaji wa Windows 10 wametumia zaidi ya masaa bilioni 11 kwenye vifaa vyao. Njia pekee ya wao kuwa na data hii ni kutokana na programu endeshaji hiyo kuwa inawatumia data mbalimbali za utumiaji.
Ingawa kuna mafanikio ya ukuaji wa utumiaji bado wengi wanaona ukuaji bado mdogo katika maeneo ya kibiashara. Na kwa kiasi kikubwa Windows 10 imefanikiwa zaidi ya matoleo yaliyopita ya programu endeshaji hiyo kutokana na hii kupatikana bure kwa wengi na pia kutokana na wengi waliokuwa kwenye Windows 8 ambayo haikupendwa sana kusasisha (upgrade) mara moja kwenda Windows 10.
No Comment! Be the first one.