Rekodi kama hii ingetegemewa kushikiliwa na kampuni kama Samsung au Apple hivi lakini amini rekodi hiyo imewekwa wiki hii na kampuni ya simu ya nchini Uchina inayokuja juu kwa kasi sana. Kampuni hii inaitwa Xiaomi na wengi wamesema kama ni kuifananisha kiubunifu basi kampuni hii inaweza pewa jina la utani la kuwa ni Apple ya Uchina.
Kampuni hii inayoshikilia namba moja katika uuzaji wa simu janja nchini Uchina imefanikiwa kuuza simu zaidi ya milioni 2 ndani ya kipindi cha masaa 12 na hivyo kufanikiwa kuweka rekodi ya dunia ya Guinness (Guinness World Record) kwa mauzo mengi ya simu katika muda mdogo zaidi.
Mauzo hayo yalifanyika katika bonanza yao ya kuadhimisha miaka mitano tokea kampuni hiyo ianzishe April 6, mwaka 2010, jijini Beijing, Uchina.
Nani alikuwa anashikilia rekodi hiyo kabla?
Ni wao wenyewe!!! Ndio, wao ndio waliweka rekodi hiyo katika kipindi kama hichi mwaka jana wakati wakiadhimisha miaka 4, kipindi hicho waliweka rekodi ya mauzo ya simu milioni 1.3 katika bonanza lao la masaa 12.
Simu janja 2,112,010, idadi kamili ya simu walizouza ndani ya masaa 12 tarehe 8 April katika Bonanza lao.
Bonanza hilo wanaliita kwa jina la ‘Mi Fan Festival’ linakuwa linahusisha mauzo ya simu zao mbalimbali kwa punguzo. Simu zao zenye muonekano mzuri na nyingi zikiwa zinatumia programu endeshaji (OS) ya kwao ambayo inatengenezwa kutumia Android, zina sifa ya kuwa za kuvutia na pia zikiuzwa kwa bei isiyo ghali sana ikilinganishwa na zile kutoka kwa Samsung na Apple.
Katika bonanza hilo kampuni hiyo pia ilifanikiwa kuuza TV 38,000 na vifaa vingine mbalimbali vingine janja hii ikiwa wanaonesha ukuaji wao kutoka kutegemea biashara ya simu tuu.
Kampuni hii imepewa sifa ya moja ya makampuni yanakua zaidi duniani na tayari imeonesha nia ya kusambaa kwa mataifa mengi zaidi zaidi ya Uchina. Kwa mwaka 2014, kampuni hii ilifanikiwa kuuza simu janja milioni 61 na kupata mapato ya takribani dola bilioni 12 za kimarekani na kuifanya kampuni hii ya Xiaomi kushika nafasa ya 3 katika makampuni makubwa ya simu janja duniani baada ya Apple na Samsung.
No Comment! Be the first one.