Ushawahi kujiuliza kama YouTube inalipa kwa mambo mengine nje ya muziki na vichekesho? Fahamu mtoto mwenye miaka 6 raia wa Korea Kusini anayefahamika kwa jina la Boram Ki amenunua jengo lenye thamani ya dola za kimarekani milioni 8 (zaidi ya Tsh bilioni 16) kwa pesa anazotengeneza kwa sababu ya YouTube.
Kwa mujibu wa habari iliyotolewa na shirika la CNN, Boram anaendesha chaneli mbili tofauti katika mtandao wa YouTube akiwa na jumla ya wafuatiliaji zaidi ya milioni 30.
Jengo hilo la ghorofa 5 lipo katika eneo la Gangnam, moja ya maeneo ghari katika jiji la Seoul nchini Korea Kusini.
Kupitia kampuni ya Boram Family iliyoanzishwa na wazazi wake amenunua jengo hilo kupitia malipo anayoyapata kupitia chaneli zake mbili za YouTube.
Katika chaneli hizo mbili za Boram Ki, moja ina wafuatiliaji milioni 13.6 na nyingine ikiwa na wafuatiliaji milioni 17.6 .
Baadhi ya video alizozisambaza kupitia chaneli hizo zimeangaliwa zaidi ya mara milioni 350. Boram huingiza dola milioni 3 kwa mwezi.
Wazazi wengi wanachagua kutumia YouTube kama sehemu burudani kwa watoto wao na hii inafanya akaunti za watoto kuzidi kupata umaarufu na video nyingi zinatazamwa kwa wingi sana. Makampuni ya utengenezaji wa vitu vya kuchezea vya watoto wanachukua nafasi hii kuingia mikataba minono na akaunti hizo.
Katika akaunti zake Boram amekuwa akiweka maudhui ya michezo ya watoto na visa kadhaa vinavyomuhusu vinavyovutia mamilioni ya watazamaji.
Kwa sasa watoto wamekuwa wakiingiza pesa nyingi kupitia Youtube. Kwa mujibu wa Forbes mwaka jana staa wa YouTube aliyeingiza pesa nyingi zaidi ni Ryan Kaji raia wa Marekani mwenye umri wa miaka saba ambaye aliingiza dola milioni 22.