Ukiwa unatazama video katika kioo cha Simu, Tablet au Kompyuta yako kwa kawaida huwa unaona upande mmoja tu, upande ambao kamera inamulika. Kwa kawaida pia ni vigumu, na mwanzo haikuwezekana kabisa kutazama upande wa nyuma ya kamera. Utaona upande ambao kamera itataka wewe utazame tu.
Lakini si kitu tena. Sasa, kupitia mfumo mpya wa kurekodi na kucheza video uliopewa jina la ‘Virtual Reality’, sasa unaweza kutazama video kutokea upande wowote uliopo, wakati wowote.
YouTube wametangaza maboresho ya aina mbili kwa ajili ya App yake ya Android kwa kuiwezesha kupanua matumizi ya video halisi, katika kuendeleza teknolojia mpya ya ulimwengu wa utazamaji.
VR zinampa mtazamaji uzoefu unaofanana kabisa na kuwepo eneo la tukio, ambapo kwa kawaida mtu huweza kugeuza shingo kutazama ama kulia au kushoto, juu au chini na sasa ukiwa na VR, utaweza kufanya hayo yote.
Ili kuweza kutazama video hizi kwa sasa, mtazamaji anaweza kutumia App ya YouTube ya simu za Android, au kutumia kisakuzi cha Google Chrome kwenye kompyuta yake. Kwa watumiaji wa IOS na visakuzi kama Internet Explorer au Mozilla Firefox, huduma hiyo italetwa siku chache zijazo, Google wameeleza.
Kutazama video hizo, watumiaji watatakiwa kufungua video ambazo zimerekodiwa katika mfumo wa nyuzi 360 (VR Mode), na kubonyeza kitufe cha VR ili kutazama kwa kuchagua vielekezi vilivyowekwa katika kioo cha simu zao.
Mtumiaji pia anaweza kutumia kifaa maalum kinachoitwa ‘VR Cardboard’ kinachokuwezesha kutazama video hizo kutoka upande wowote atakaotaka kujivinjari. VR Cardboard zinapatikana kwa gharama za kati ya $5 na $50.
Kwa kufanya hivi, mtazamaji anaweza akapata uzoefu wa kutazama filamu kupitia miwani zenye mfumo maalum wa 3D. VR ni teknolojia iliyotazamiwa zamani kutolewa baada ya mfumo wa 3D, na sasa wamefanya hivyo.
Unaweza kutazama mfano wa video hizi kwa kubonyeza hapa au tazama filamu ya The Hunger Games VR Mode kupitia App yako ya simu au bonyeza hapa .
Chazo cha Makala haya ni mtandao wa Reuters, Youtube Liveblog, na TheNextHome.
One Comment