Shirika la utangazaji la Zanzibar ZBC limetangaza kusitisha matangazo ya Televisheni na Radio katika mfumo wa Analogia na kwenda katika mfumo wa Digitali.
Shirika hilo limesema litazima mitambo ya Analogia siku ya Alhamisi ya tarehe 31 Agosti 2017 na kuingia katika mfumo wa kisasa wa Digitali.
Kufuatia hali hiyo shirika hilo la habari limewataka wananchi wote wa Zanzibar kununua king’amuzi kitakacho wawezesha kuona matangazo ya Televisheni ya ZBC na radio.

Katika hotuba yake katika maadhimisho ya miaka 53 ya Mapinduzi ya Zanzibar, Rais Ali Mohamed Shein alisema, “Katika kuliimarisha Shirika la Utangazaji la Zanzibar (ZBC), Serikali, mnamo mwezi wa Novemba, 2016, imenunua vifaa vipya vya kisasa na mitambo kwa ajili ya ZBC TV na Radio. Vifaa hivyo vinatarajiwa kufika nchini hivi karibuni.
Vile vile, vifaa mbali mbali vimeagizwa pamoja na ving’amuzi vipya na vya kisasa kwa ajili ya mitambo ya digitali ya ZBC TV. Kwa kupatikana vifaa hivyo, ZBC wataweza kuzima, mitambo ya “Analog” kuanzia Aprili mwaka huu.
Aidha, jengo la “Karume House” na jengo la ZBC Radio yameanza kufanyiwa matengenezo makubwa ili yalingane na vifaa vitakavyowekwa.”
Tanzania bara kupitia mamlaka ya mawasiliano TCRA mwaka 2012 Desemba 31ilizima mitambo ya Analogia na kwenda Digitali. Zoezi hilo lilikwenda kwa awamu kwa baadhi ya mikoa kabla ya kuzima nchi nzima.