Wengi wanajiuliza Chromebook ni Laptop za aina gani na ni kipi hasa kinazitofautisha laptop hizo na zingine? Kaa mkao wa kula kwani leo TeknoKona imejipanga kukutajia tofauti zake na kulinganisha na zile za kawaida.
Cha kwanza kabisa kinachotofautisha kompyuta hizi ni programu endeshaji yake. Hizi huwa zinaendesha na programu endeshaji spesheli kutoka Google yaani Google Chrome OS ambayo ni tofauti kabisa na Wondows OS na Mac OS.

Moja ya sifa nyingine kubwa ya kompyuta hizi ni kwamba zimetengenezwa makusudi kabisa ili zitumike kwa urahisi zikiwa zimeunganishwa na huduma ya intaneti (kwa lugha nyingine ni kwamba utakuwa unafurahia kuitumia zaidi ukiwa na huduma ya intaneti) kwani App zake nyingi na baadhi ya document zinaishi katika uhifadhi wa mtandaoni.
Kutokana na sababu hizo (baadhi) ndio maana unakuta laptop hizi hazina ujazo mkubwa sana wa uhifadhi na la kuvutia (kushangaza!) zaidi ni kwamba hazina gharama kubwa ukilinganisha na laptop za kawaida ambazo tuna(tume)zitumia sana.

Bila kusahau sifa yake nyingine kubwa (pengine kubwa kushinda zote) ni kwamba laptop hizi zinahifadhi chaji kwa kipindi cha muda mrefu – inaweza ikakaa na chaji kwa siku kadhaa kwa matumizi ya kawaida – sana.
Nafikiri uwezo wa kukaa na chaji kwa muda mrefu, bei ya chini ni moja kati ya vitu ambavyo vinaweza vikamfanya mtu yeyote kukimbilia kununua laptop hizi.
Zifuatazo Ni Sifa Zake Zingine.
RAM: inapokuja katika swala zima la Chromebook RAM ya uwezo wa 2GB unafaa kabisa japokuwa kuna matoleo mengine yanenda hadi RAM ya 4GB. Ni sawa kabisa unaweza ukachagua hiyo yenye RAM ya GB4 kama una matumizi makubwa kidogo katika Laptop hiyo.
CPU: hapa ndio unaweza pia ukaangalia ufanisi wa Laptop hizo. Hapa kuna aina nyingi za CPU ambazo kati ya hizo unaweza ukachagua kompyuta ambayo ina CPU ile unayoitaka. Kwa mfano kama unataka laptop yenye kasi (spidi) kubwa wakati unafanya mambo yako basi chagua ile yenye CPU ya Core i3 na achana na ile yenye CPU ya Intel Celeron.
UJAZO: hapa ndio kimbembe kwa baadhi ya watu, najua wengine mtaanza kujiuliza kama je hii ni simu au laptop?. Chromebook zinakuja na ujazo wa angalau GB 16 za uhifadhi. Kumbuka laptop hizi hazijatengenezwa spesheli kwa ajili ya kuhifadhi App na mafaili yenye ujazo mkubwa. Kuna zingine zinakuja na sehemu ya ‘SD Card Reader’ hii inamaanisha unaweza ukaongeza ujazo huo mpaka kufikia GB 64 (ambazo bado ni ndogo kwa baadhi ya watu). Lakini cha muhimu kumbuka kwamba mambo mengi yanafanyika katika mtandao.
KIOO: Chromebook yenye kioo kidogo kabisa inakuwa na kioo cha pixel 1366 x 768. Lakini kama unataka kile cha kuonyesha picha, video na ‘graphics’ vizuri basi huna budi kuchagua Chromebook yenye kioo cha HD chenye pixel 1920 x 1080.
Kumbuka kuna baadhi ya Chromebook zinawezesha kutumia App za Android kutuka Google kwa mfano ‘Asus Chromebook Flip’. Hebu fikiria App zote zile katika laptop yako. Kwa Chromebook zingine ambazo bado hazijawa na uwezo huo wa kutumia App za Android nao pia wakae mkao wa kula kwani katika siku za usoni wataweza kufanya hivyo.

Chromebook ni laptop ambazo zinatengenezwa na makampuni mengi sana. Kuna Asus, Hp, Lenovo, Toshiba, Dell na makampuni mengine kibao yanayotengeneza hizi.
Cha msingi ni kujiuliza kuwa unanua laptop hizo kwa kazi gani na nani unamnunulia kabla ya kuzinunua.
Niandikie hapo chini sehemu ya comment sifa nyingine kubwa ambayo sijaitaja au ambayo wewe unaipenda zaidi katika Laptop hizi ambayo inazitofautisha na laptop zingine.